CORE Securities Limited na Exim Bank kushirikiana katika Uwakala wa Hisa na Dhamana

DAR ES SALAAM, Tanzania

Biashara ya Hisa na Dhamana imechukua ukurasa mpya nchini baada ya Exim Bank na  Wakala wa Masoko ya Hisa na Dhamana, CORE Securities Limited kukamilisha mipango ya kuunganisha shughuli zao katika Masoko haya na sasa wakisubiria baraka za Tume ya Ushindani wa Biashara.

Muungano huu utazifanya kampuni hizi kuwa na uwezo mkubwa wa kiushindani katika Masoko ya Hisa na Dhamana kwa sababu ya Mtaji kuongezeka na matawi yaliyoenea vizuri kiushindani ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, George Fumbuka, Exim Bank itanunua asilimia 80 ya kampuni ya CORE Securities ili kuimarisha uwezo wake wa kiushindani na kusambaza huduma zake kiurahisi.

“Ununuzi umezingatia masuala mawili. Kwanza ni mtaji mpya unaohitajika na pili ni mtandao mzuri wa matawi  – Exim ina yote hayo,” alisema.

Alisema hamu kubwa ni kufikia wateja wengi kote nchini na kwa kuunganisha na Benki ya Exim, wataongeza ufikishwaji wa huduma katika sehemu nyingi, ambayo ni karibu matawi 30 nchini na matawi mengine sita nchini Comoro, Djibouti na sasa Uganda.

Mkurugenzi Mtendaji alisema kuwa Uwakala wa Masoko ya Hisa na Dhamana umebadilika ambapo kwa sasa Mawakala sio tu watoa huduma, bali pia hununua Hisa za Awali (IPO) na kuziuza mara thamani inapoongezeka. Alisema kuwa hicho ndicho kilichotokea wakati wa IPO ya Vodacom ambapo karibu asilimia 95 ya hisa zote zilinunuliwa na taasisi na hasa Mawakala wa kigeni wa Masoko ya Hisa na Dhamana.

“Tunahitaji mfuko wa ziada ili kuwezesha kununua hisa wakati wa IPO … na pia ada ya leseni imepanda kwa siku za hivi karibuni,” Bwana Fumbuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Mshindi wa Tuzo ya Wakala Bora Afrika Mashariki mwaka 2013 alisema.

Kwa mujibu wake, hapo awali kuwa Wakala wa Masoko ya Hisa na Dhamana zilihijitajika shilingi milioni 20 lakini leo zinahitajika dola za kimarekani 500,000 takribani shilingi bilioni 1.10. Kiwango cha Tanzania ni cha chini ikilinganishwa na Kenya dola za Kimarekani 800,000 (1.2 bilioni), Nigeria dola za kimarekani milioni 1.0 (2.2 bilioni) na Afrika Kusini dola za kimarekani milioni 2.0  (4.4 bilioni).

Hata hivyo, mpango mzima haujajulikana bado na hautaweza kupita bila kupata baraka za Tume ya Ushindani (FCC). FCC jana ilitoa idhini ya umma kutoa maoni ya wadau kuhusu ushirikiano huu.

“FCC kwa sasa inachunguza ushirikiano unaotarajiwa kulingana na  Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 na Kanuni za Ushindani za mwaka 2013,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa Zaidi: Dar bank plans to buy stock brokerage firm

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *